Azam FC shujaa kombe la Mapinduzi
Kivumbi cha mashindano ya kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar kimemalizika rasmi usiku wa kuamkia leo, kwa kikosi cha matajiri wa jiji la Dar es Salaam Wanalambalamba Azam FC kunyakua ubingwa huo kwa kuwatungua Jamhuri ya Pemba kwa bao 3 kwa 1 kwenye fainali. 

Baada ya kuwaondosha vigogo Simba na Yanga kwenye mashindano hayo kwa nyakati tofauti, Azam walitinga fainali kwa mbwembwe, na kucheza fainali hizo katika uwanja wa Amaan jana katika kuadhimisha sikukuu ya Mapinduzi ya visiwa hivyo yaliyofanyika miaka 50 iliyopita.
Jamhuri FC ndio waliokuwa wa kwanza kujiandikia bao kupitia kwa nyota wao Ally Idd katika dakika ya 18, kabla ya mfungaji bora wa kikosi cha Azam John Boko kuisawazishia timu yake katika dakika ya 42.
Baada ya mabao hayo hatimaye kandanda lilisakatwa vikali kwa timu zote mbili kushambuliana, hadi dakika za majeruhi katika dakika ya 87 pale Kipre Cheche kutoka Ivory Coast alipoiandikia Azam bao la pili na kiungo Mrisho Khalfan Ngasa kuhitimisha kwa kutandika bao la 3 dakika 2 baadaye.
Hapo awali vikosi vya Simba na Mafunzo ya Zanzibar vilifanikiwa kutinga nusu fainali ya mashindano hayo, kabla ya kutolewa na timu hizi zilizocheza fainali, na kwa mujibu wa taratibu za mashindano hayo hapakuwa na mchezo wa kumtafuta mshindi wa tatu.
Top Stories »





