CUF kwawaka, Hamad afukuzwa
Mkutano wa Halmashauri kuu ya Chama Cha Wananchi CUF umefanyika hii leo visiwani Zanzibar, ukiwa na ajenda kuu ya kujadili kile kilichoelezwa baadhi ya wajumbe wake kukihujumu chama kwa kuongozwa na Mbunge wa Wawi Hamad Rashid na wajumbe wenzake 13, na kuhitimishwa kwa Hamad na wajumbe wengine watatu kufukuzwa. 

Taarifa kutoka katika mkutano huo imeeleza Hamad ametuhumiwa kuendesha mikutano ya kukihujumu chama kwa kutaka kugombea nafasi ya ukatibu mkuu, bila kukijulisha chama.
Taarifa zaidi imeongeza kuwa Hamad alipaswa kufuata taratibu katika kufanya masuala hayo, kwa kuwa chama hicho kinaendeshwa kwa taratibu na sheria za kikatiba.
Naye Hamadi akijibu hukumu hiyo, amesema tayari amekwenda mahakamani na kuchukua hati aliyomkabidhi katibu mkuu Seif Shareef Hamad, ikiweka pingamizi la chama hicho kumvua uanachama.
Amekiri wazi kuweka nia yake bayana ya kugombea nafasi inayoshikiliwa na Seif ili kumng’goa madarakani, na kulalama hakuna uwazi katika chama hicho, huku akieleza uamuzi wa Kikao hicho kumfukuza si sahihi hata kidogo.
Hamad ambaye ana wafuasi wengi Tanzania Bara wanaomuunga mkono katika sakata hilo, amefukuzwa sambamba na Juma Said, Shoka Hamis, Doyo Hassan Doyo na Juma Sanani.
Kabla ya kuanza kwa kikao hicho kilichohudhuriwa na wajumbe 51 kati 60 waliotarajiwa kuwepo ukumbini, Wanahabari waliruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi na kupiga picha kwa muda wa dakika 5, kabla ya kutolewa nje na kuahidiwa kupewa matokeo ya mkutano huo mara tu baada ya kuhitimishwa.
Hali ya wasiwasi iliwakumba baadhi ya wajumbe ambapo mahojiano yalianza moja kwa moja kwa kuhojiwa baadhi ya watuhumiwa.
Hata hivyo hali ilikuwa tulivu na ulinzi kuimarishwa katika eneo lote la mkutano, kuzuia hali yoyote ya uvunjifu wa amani baina ya wajumbe wanaotofautiana katikab kisa hicho.
Hamad Rashid akiungwa mkono na wajumbe wengi kutoka Tanzania bara, aliingia katika mgogoro na Katibu mkuu wa Taifa wa Chama hicho na Makamu wa kwanza wa Raisi wa Zanzibar Maalim Seif Shareef Hamad, kwa kutangaza azma ya kutaka kugombea kiti cha ukatibu ukuu kumng’oa Maalim Seif.
Kutokana na hali hiyo propaganda za wawili hao zilianza kusambaa kwa kila mmoja akielezwa kutetea upande wake, hali iliyopelekea kupigana kwa baadhi ya wafuasi wa pande hizo mbili katika maeneo ya Tanzania Bara.
Top Stories »





