Diamond sokoni tena na “lala salama”
Nyota wa muziki wa kizazi kipya jijini Dar es Salaam Naseeb Abdul Jumaa ‘Diamond’, ametangaza rasmi kushusha Albam Mpya sokoni inayofahamika kwa jina la “Lala Salama”, ikiwa na jumla ya nyimbo 10 huku akiahidi nyimbo nyingine za ushirikiano (collaboration) na wasanii wa Kimataifa katika siku za usoni. 

Mojawapo ya nyimbo alizozitaja katika albamu hiyo mpya ni pamoja na ‘Kwa nini’, ‘Chanda chema’, ‘Kizaizai’, ‘Darasa’ pamoja na ‘nimpende nani’ miongoni mwa nyingine.
Nyota huyo ambaye pia ni mchumba wa aliyewahi kuwa mlimbwende wa Tanzania Wema Isaac Sepetu, amekuwa na mafanikio makubwa katika msimu wa mwaka uliopita, akirindima katika kugonga maonyesho (show) katika maeneo tofauti zikiwemo ziara za nje ya nchi kama vile Uholanzi, Sweden, Italia na Uingereza, na kueleza siri kubwa ya mafanikio hayo ni kujituma.
“sina zama za ujuaji, najituma sana katika kazi zangu na kuomba ushauri kwa watu…kuleta mambo mapya kila siku kwa mashabiki wangu.”amebainisha msanii Diamond
Moja ya tofauti katika utenngenezaji wa albamu hiyo imeelezwa kuwa nyingi ya nyimbo zake zimerekodiwa katika studio tofauti na ile iliyozoeleka ya (Sharobaro records), lakini msanii huyo amekana kuwa na matatizo na studio hiyo, na kwamba bado ana mahusiano mazuri na mmiliki wa studio hiyo Bob Junior.
Aidha nyota huyo ameeleza kutumia kiasi mwaka mmoja tangu aanze kuishughulikia albamu hiyo, hadi alipoitoa hadharani mwishoni mwa mwezi uliopita, ikiwa na mchanganyiko wa nyimbo za mahadhi ya R&B, Afro-pop, Bongo Flavor na mengine.
Top Stories »





