Hamad: Sihamii kwingine, nitaanzisha changu
Baada ya uamuzi wa Chama Cha Wananchi CUF kumfuta uanachama wake Mbunge wa Wawi Hamad Rashid, mbunge huyo ameibuka na kusema bado yeye ni mbunge wa CUF kufuatia amri ya mahakama, na kwamba kama atalazimika kuondoka hatajiunga na chama kingine chochote. 

Kiongozi huyo wa zamani wa Kambi ya upinzani Bungeni kupitia CUF, amekaririwa akiyaeleza hayo kwa vyombo vya habari leo, alipoulizwa kuhusumustakbali wake kisiasa pasipo CUF.
Hamad amesisitiza kuwa uamuzi wa chama chake bado si amri ya kuzingatia, na kwamba ni mwanachama halali wa chama hicho, kutokana na pingamizi lililowekwa na Mahakama kwa uongozi wa CUF.
Ameongeza kuwa suala lililopo kwa sasa ni yeye kukaa na wananchama wenzake na kujadili hali hiyo, hususani kuhakikisha kuwa anaendelea kuiimarisha CUF iliyo bora, na kama itashindikana, basi ataanzisha chama kingine.
Taarifa kutoka katika matawi mbalimbali ya CUF kwote nchini imeelezwa kuwa ya pande mbili, baada ya baadhi ya wanachama wanaomuunga mkono mbunge hususani katika maeneo ya Tanzania bara, kurudisha kadi na kusubiri uamuzi wa kiongozi huyo.
Baadhi ya maeneo yaliyobainika kurudisha kadi za CUF ni pamoja na Tanga ambapo zaidi ya wanachama 100 wameripotiwa kurudisha kadi mara tu walipopata habari kuwa Hamad Rashid ameachishwa uanachama, na pia wanachama wengine jijini Dar es Salaam kufuatia, huku tishio kubwa zaidi likielezwa kuwa mkoani Mwanza kunakoaminika kumuunga zaidi mkono mbunge huyo.
Katika kikao cha Halmashauri kuu ya CUF kilichoketi jana mjini Zanzibar, palifikiwa uamuzi wa kumsimamisha mbunge huyo uanachama pamoja na wajumbe wengine wanne wa Kamati kuu, kwa madai ya kuendesha kampeni za kutaka kumg’oa katibu mkuu wa sasa aliye Makamu wa kwanza wa Raisi Zanzibar Maalim Seif Shareef, hali iliyoelezwa kuwa ni ya kukivuruga chama.
Top Stories »





