Hatma ya Hamad Rashid CUF mashakani
Mgogoro baina ya Mwenyekiti wa zamani wa kambi ya upinzani Bungeni na mbunge wa Wawi Zanzibar Hamad Rashid Hamad na Katibu mkuu wa CUF Taifa Maalim Seif Shareef Hamand umefikia pagumu, baada ya Kamati ya Maadili ya chama hicho kushindwa kumhoji kiongozi huyo. 

“Nimeikataa kamati iliyotumwa kunihoji maana tayari ilishanihukumu” ni Mbunge Hamad Rashid akieleza hayo jana, ambapo aliwatuhumu wajumbe watano kati ya nane waliounda kamati hiyo, akisema kuwa hana imani nao na kwamba waliunda njama za kutaka afukuzwe kwenye chama.
Mbunge huyo wa Wawi aliingia kwenye mgogoro na Katibu wake mkuu Maalim Seif baada ya kutangaza nia ya kuogombeaa kiti hicho cha ukatibu wa Chama, hali ambayo ilionekana kupingwa na Maalim Seif na kuzua tafrani baina yao ambapo sasa Hamad Rashid anatuhumiwa kukihujumu chama.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka CUF, mkutano huo wa Kamati ulikuwa ufanyike jana asubuhi na kwamba mbunge huyo hakuingia kuhojiwa kwa madai hayo kuwa wajumbe hao wasingemtendea haki.
Hata hivyo ujumbe wa Kamati hiyo ulieleza kuwa ulipewa jukumu la kumsomea mbunge huyo mashitaka yanayomkabili tu, na si kutoa hukumu.
Kutokana na hatua hiyo, Hamad sasa huenda akajadiliwa moja kwa moja katika mkutano wa Halmashauri kuu ya Chama hicho utakaofanyika mwishoni mwa juma.
Top Stories »





