News / Articles / Kwa Alshabab, Kenya imevamia msitu kwa kiwembe

image

Kwa Alshabab, Kenya imevamia msitu kwa kiwembe

By dar411

Kuna methali inayosema” jambo usilolijua ni kama usiku wa kiza” halafu wahenga wakarudi kusema “kwa mwoga hakiendi kilio”. ni jambo la kuogofya kuoga maji usiyojua kina chake kwa kuwa tahamaki waweza kuzama. image

image

Kikundi cha “Alshabab” kinachoaminika kuwa na mafungamano na kile cha kigaidi duniani Alqaeda, hakina maskani maalumu, japokuwa kina maeneo ya kuratibia mashambulizi yake na kufunza wapiganaji wapya katika eneo la Kusini mwa Somalia karibu na mpaka wa Kenya.

Ni kikundi ambacho hakimiliki nyumba, au biashara halali, eneo la ardhi au mali inayotambulika; na kimsingi hawana dhamana na hawatambuliki kwa kutazama.

“Mtu wa Alshabab hana mark (alama) usoni, na wanaongea Kiswahili sawa na Wasomali wanaoishi Kenya” alisema mama mmoja wa Kenya mara baada ya shambulizi la guruneti jijini Nairobi.

Hisia za uwepo wake ni pale unapopata taarifa kuwa watu fulani wametekwa na haijulikani walipo, au linaporushwa bomu mahali fulani na kuua; hapo ndipo unapotambua kuwa ni Alshabab wamefanya kazi hiyo, kwa kuwa mara nyingi hujibu kwa ujumbe kuwa sisi (Alshabab) tunahusika.

Sawa na Alqaeda, Alshabab wanaratibu shughuli zao kwa namna tatu: Kwanza kuna watu maalumu wanaotathmini na kuratibu mashambulizi (officials), kisha kuna kundi linaloandaa silaha za kutumia na tatu ni kundi la mwisho la kuendesha mashambulizi.

Wengi wa watu hawa huishi misituni na hujivika nguo ndefu na kufunika nyuso kwa vitambaa, lakini wanapotoka nje na kuingia kwenye maeneo ya watu (public areas) huvaa kawaida na huweza kuishi popote bila kutambulika hadi pale anapofanya tukio.

Wakati mwingine wanaweza kuendesha mashambulizi ya waziwazi dhidi wapinzani mfano majeshi ya Serikali wakiwa wamefunika nyuso, na mara nyingi mawasiliano huwa kwa njia ya mitandao pekee mara wanapotoka misituni na maeneo ya kufanyia mazoezi, na kila mmoja anatambua wajibu wake.

Je, moto uliowashwa na Jeshi la Kenya unaweza kuzimwa kwa kuingia ndani ya Somalia? maana suala limekaa kimaigizo, Majeshi ya Kenya yanaingia Somalia, wakati huku nyuma vikundi vya Alshabab vinapenya kuingia Kenya kimyakimya; maji haya Kenya itayaoga?

Katika hili kuna hatari pia vikundi vingine vilivyoko nje ya Kenya na Somalia vikaingia Kenya kuisaidia Alshabab

Alshabab imekuwepo kwa muda mrefu katika kupambana na Serikali halali ya nchi hiyo, na kutanua uwigo wake kwa kuteka watu maeneo ya mpakani na kudai fidia ya fedha kwa ndugu za watekwaji, pamoja pia na kufanya uharamia wa kuteka meli kwenye ukanda wa bahari ya Hindi. Yote haya ni kwa ajili ya kujipatia kipato cha kuendeshea shughuli zao.

Serikali ya Jamhuri ya Kenya sasa imeamua kukata shauri, na kupitisha uamuzi wa kutumia Jeshi lake kuingia ndani ya Somalia kuwasaka Alshabab na hasa ikilenga kuharibu vyanzo vyake (maeneo wanayoratibia mashambulizi na kuwafunzia wapiganaji wapya).

Kilichotokea muda mfupi baadaye, ni kikundi hicho kutangaza vita mpya dhidi ya Kenya na kuapa kufanya mashambulizi ya kutosha ndani ya Kenya.

Cha kufahamu ni kwamba wafuasi wa kikundi hicho wametapakaa kila upande na si Kenya peke yake, na kwa kuwa hawana alama usoni, wanatumia muda wao kusoma mazingira na kupanga namna wanavyoweza kufanya shambulizi, hasa baada ya kufanikiwa kuingia na silaha.

“Tunaishi na Wasomali wengi, wengi wanafanana na Wakenya, na Wakenya wanafanana na Wasomali” ameelza mkazi mmoja na jijini Nairobi na kuongeza “Pia Wakenya wengi wanaingia Kusini mwa Somalia na huwezi kuwatofautisha watu hawa” amemaliza mkazi huyo

Nchi ya Kenya ina watu wengi wenye asili ya Somalia wengi pia wana uraia halali wa Kenya, wengine wakiwa wanatoroka katika kambi za wakimbizi na kuingia maeneo ya kati ya Kenya. Lakini Wanaalshabab pia hutapakaa kwa njia hiyohiyo kwenye maeneo mengine.

Kwa mujibu wa Katibu mkuu wa usalama wa ndani wa Kenya Francis Kimemya, hatua zimekuwa zikichukuliwa kukabiliana na wimbi la kutoroka kwa wakimbizi kambini na kuingia maeneo ya raia, na kwamba Polisi huwakamata na kuwarudisha kambini, lakini bado Wasomali wengi wako katikati ya Wakenya.

Jumanne iliyopita shambulizi la guruneti lilirushwa kwenye mgahawa mmoja pembezoni mwa jiji la Nairobi, kabla ya bomu kurushwa kwenye kituo cha basi saa chache baadaye na kuua mtu mmoja huku wengine wakijeruhiwa katika mashambulizi yote na kulazwa katika Hospitali ya JomoKenyata Nairobi.

Hali kadhalika hali ilizidi kuwa tete baada ya Alhamisi mchana shambulizi kufanywa dhidi ya gari ndogo na kuua watu wanne na kujeruhi wengine wanne umbali mdogo kabla ya kufikia mpaka wa Somalia kwa kutokea Kenya.

Hii ni kutokana na ripoti kutoka Jeshi la Kenya kupitia vyombo vya habari vya nchi hiyo na vile vya Kimataifa kikiwemo kituo cha habari cha Uingereza BBC.

Hata hivyo siku moja baadaye Jeshi la Kenya lilifanikiwa kumkamata raia mmoja mwenye asili ya Kenya wakimshuku kuwa mhalifu, na walipopekua nyumba yake waligundua kuwepo mabomu ya kurusha kwa mkono (guruneti) 13 , risasi pamoja na bunduki nzito na zile za rashasha.

Maofisa wa usalama wa Kenya wanasema wanamshikilia mtu huyo, lakini wakajizuia kueleza kama ni mfuasi wa Alshabab, wakidai kuwa kwa uchunguzi wao anaonekana kutohusika na matukio yaliyotokea hivi karibuni, lakini wakakiri kuwa silaha zake zitakuwa zimeingizwa kutoka Somalia kwa kuwa maghala ya Jeshi la Kenya hayana silaha za aina hiyo.

Kuna taarifa zisizothibitishwa kutoka Kenya kuwa kijana huyo amekubali kuhusika na operesheni za Alshabab.

Wakati huo huo malalamiko makubwa yametolewa na wakazi wa maeneo ya Kenya wenye asili ya Somalia, wakidai kunyanyaswa na Polisi kwa ukaguzi, Lakini Polisi imejibu kuwa inahakikisha kila raia ana uhalali wa kuwepo alipo na kwamba mkimbizi yeyote atarudishwa kambini.

Pengine Jeshi hilo halikufahamu jinsi mtandao wa kikundi hicho ulivyoenea, ama hawakutambua nguvu na uwezo ambao wangeweza kuutumia kuihujumu Kenya, au pengine walitambua yote lakini wakapuuzia.

Waswahili wanasema “maji ukishayavulia nguo sharti kuyaoga”. Kenya imeingia kwenye mgogoro na Wapiganaji hawa ambao wanaweza kuishi popote na kufanya mashambulizi kwa yeyote.

Serikali ya Kenya inapaswa kukaa upya na kufikiria jinsi inavyoendesha operesheni hiyo, na kutathmini vilivyo idadi ya waweka usala iliyoko nao na jinsi ya kuwaingilia na kuwaharibia mipango yao ndani ya Kenya, kisha ishirikiane kwa karibu na mataifa jirani hususani Somalia yenyewe, kuweza kukabili maskani yao.

Mkanganyiko pia umetokea na kuiweka Kenya mahali pagumu, pale Serikali ya Somalia ilipotoa taarifa kuwa haijakubaliana na Kenya kuwaruhusu wanajeshi wake kuingia kwake na kuwasaka Alshabab.

Akijibu hoja hiyo, Katibu usalama wa Kenya Kimemya amesema ni jambo la kushangaza kwa kuwa kila kitu kilikuwa wazi. Taarifa za hivi punde zimeeleza tayari Serikali ya Kenya imetuma ujumbe Somalia kuitaka Serikali hiyo kuthibitisha usemi wake kuwa haina makubalino na Kenya juu ya operesheni hiyo.

Kwa mujibu wa ujumbe uliotumwa na Alshabab, mashambulizi zaidi yamepangwa kufanyika ndani ya Kenya, na kwa kuwa watu hao hawana alama, inawezekana wametapakaa kila mahali nchini humo, ni rahisi mno kuzua majanga.

Wengi watakaoathirika ni raia wasio na hatia, kwa kuwa wapiganaji hawa kama ilivyo sera ya ugaidi hulenga maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi, taasisi, maeneo ya kuabudia, shule, hospitali, vituo vya basi, katikati ya miji na kwingineko.

Wakati huo huo, “mwenzako akinyolewa na zako tia maji” ni usemi wa mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania Inspekta Jenerali Saidi Mwema akizungumza na vyombo vya habari Jumatano wiki hii, na kubainisha kuwa Polisi wamejipanga kisawasawa kulinda raia wake.

Mwema aliongeza kuwa Jeshi hilo limeweka doria ndani na katika mipaka ya nchi hususani pia ukanda wa bahari, na kwamba litawasiliana na askari wa nchi jirani kupeana taarifa za kudhibiti uhalifu wowote.

 
image
image
This text will be replaced
image