Kutoka ulemavu, Ubunge hadi umauti
Licha ya ulemavu wake Regia Estelatus Mtema alifanikiwa kuingia katika orodha ya viongozi wa Taifa kama mbunge, akiwawakilisha wananchi kwa ustadi, na kujizolea umaarufu uliopotea ghafla alipopata ajali mwishoni mwa Juma, na sasa ameagwa rasmi leo Kanisani huko Tabata kwa ajili ya mazishi keshokutwa. 

Marehemu Mtema ameagwa leo katika ibada maalumu iliyoendeshwa kwenye Kanisa Katoliki la Segerea huko Tabata jijini Dar es Salaam, ambapo ndugu jamaa, marafiki na viongozi wenzake wamekuwepo kutoa heshima za mwisho.
Hata hivyo taarifa zaidi zimebainisha kuwa huduma ya kuuaga mwili wa marehemu itafanyika kwa ukamilifu kesho Jumanne Januari 17, 2012 nyumbani kwa baba yake mzazi Tabata Chang’ombe, na kwamba mazishi yake yatafanyika siku ya Jumatano katikati ya wiki wilayani Ifakara mkoani Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge Bi Anne Makinda, Kamati ya uongozi ya Bunge itakaa leo kujadili jinsi ya kuendesha mazishi ya mbunge huyo wa viti maalumu kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo.
Itakumbukwa baada ya ajali hiyo iliyotokea hapo juzi Jumamosi tarehe 14 Januari, 2012 majira ya saa 5.00 asubuhi, Viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliitisha mkutano wa dharura mara moja saa chache baada ya ajali, kujadili namna ya kuendesha msiba huo wa mbunge wao huyo.
Marehemu Regia Mtema alipoteza maisha katika eneo la Ruvu darajani mkoani Pwani, wakati gari alilokuwa akisafiria pamoja na ndugu wengine saba aina ya Toyota Landcruiser VX kupata ajali na kupinduka, wakati lilipokuwa katika jitihada za kukwepa gari lililokuwa linatokea mbele yake baada ya kulipita gari jingine (overtake).
Imefahamika kuwa abiria hao wengine waliokuwa wakiendeshwa na mbunge huyo walijeruhiwa na wanaendelea kupata matibabu katika hospitali na Tumbi Pwani. Vyanzo vya awali vimeripoti huenda marehemu (ambaye alikuwa dereva) alipata ugumu wa kufanya maamuzi ya kusimama au kukwepa gari hilo jingine kutokana na kuwa na mguu mmoja pekee wa kushoto, uliompa shinda katika kutumia pedeli za gari kwa haraka baada ya mshtuko wa kukutana na gari jingine.
Top Stories »





