Matokeo DRC tete, maandamano yaanzia London
Wasiwasi umetanda upya katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, baada ya upinzani kupinga matokeo ya uraisi uliotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo Ijumaa iliyopita, kwa madai kuwa ulijaa udanganyifu na wizi wa kura. 

Tayari kujibu hoja ya malalamiko ya wapinzani, maandamano makubwa yamefanyika katika jiji la Londoni nchini Uingereza, kwa wananchi kutoka Congo wanaoishi nchini humo kukusanyika kupinga hatua ya tume hiyo kumpa ushindi Raisi Joseph Kabila.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Sauti ya Amerika, Taasisi ya uangalizi kutoka nchini Marekani inayofahamika kwa jina la Carter, imefahamisha kuwa kura za vituo vipatavyo 2,000 kutoka jijini Kinshasa zimepotea, katika wakati ambao inaaminika kuwa mji huo mkuu Kinshasa ndiyo ngome kuu ya wafuasi wengi wa mpinzani wa Kabila Etienne Tshisekedi.
Katika matokeo hayo Raisi Kabila alijipatia ushindi mdogo wa 49% katika wakati ambao mgombea wa upinzani kupitia chama cha UDPS anayeungwa mkono na wafuasi wengi Etiene Tshisekedi amejipatia kiasi cha 33%.
Mgombea huyo amekataa kuyakubali matokeo hayo, na kueleza kuwa uchaguzi huo ulighubikwa na hila mbalimbali, huku wizi mkubwa ukifanyika kumpatia ushindi Raisi aliyeko madarakani.
Aidha mgombea mwingine wa uraisi aliyefuatia katika uchaguzi huo Vital Kamerhe, naye amelalama kuibwa kwa kura na kupendelewa kwa raisi Kabila, na kueleza msimamo wake kuwa anamuunga mkono mshindi wa pili Etienne Tshisekedi.
Maandamano zaidi yamepangwa kufanyika nchini Congo, katika hatua ya upinzani kushinikiza kubatilishwa kwa matokeo hayo yaliyompa Raisi Kabila ushindi.
Wakati hali ya taharuki ikilighubika Taifa hilo lenye eneo kubwa zaidi la ardhi barani Afrika, waandamaji wapatao 43 wamekamatwa na kuwekwa kizuizini nchini Uingereza, baada ya kusababisha fujo zilizopelekea uharibifu wa maduka na magari wakati wa maandamano, ambapo pia waandamanaji walifunga barabara.
Top Stories »





