News / Articles / Miaka 50 ya uhuru, tujivunie nini?

image

Miaka 50 ya uhuru, tujivunie nini?

By dar411

Tangu Serikali ya Tanganyika ijipatie uhuru wake mnamo Desemba 9, 1961 kisha kufanya muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964, Taifa jipya Tanzania lilipita katika misukosuko lukuki kuliko hata changamoto tunazozishuhudia hivi sasa. image

image

Serikali ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilikumbwa na matatizo makubwa matatu; kwanza iliingia katika mkakati wa kibarua kizito cha kuanza kuwaunganisha wananchi waliogawanywa na ukoloni, kisha kuanza kuijenga nchi upya kuanzia makazi, miundombinu, shule, hospitali, viwanda, mashamba na vinginevyo, kwani baada ya mkoloni kutoka Taifa lilibaki kama yatima, na ujenzi ulianzia pale, licha ya kuwa baadhi ya vitu kama vile barabara, hospitali na shule viliachwa lakini ni kwa uchache.
Mtihani wa pili ni sakata la uhaba wa mafuta (oil crisis) 1973 ambalo lililotokana na uamuzi wa nchi za OAPEC (nchi za Kiarabu wazalishaji wa mafuta) kusitisha uzalishaji wa mafuta kwa lengo la kuiadhibu Marekani na nchi nyingine za Magharibi kwa kuisaidia Israel katika vita vyake dhidi ya Muungano wa nchi za Kiarabu zilizopigana nao mwaka 1973.
Itakumbukwa mnamo Octoba 6-26 mwaka 1973, Taifa la Israel liliingia tena katika mgogoro wa vita baina yake na Muungano wa vinara wa Kiarabu Misri na Syria, wakiungwa mkono na Jordan, Lebanon, Iraq, Yemen, Saud Arabia, PLO, Algeria, Libya, Tunisia, Kuwait na Morocco japo baadhi ya hawa hawakushiriki moja kwa moja bali kwa kuchangia zana, askari na mahitaji mengine.
Hali hii ilizorotesha vikubwa hali ya uchumi wa duania, na athari kubwa ilitathminiwa kuzidi barani Afrika, ambapo nchi nyingi zilionja moja kwa moja athari hizi. Tanzania chini ya Nyerere, ilibeba mzigo mzito kukabili uhaba huu wa mafuta.
Suala la tatu ni Vita baina ya Tanzania na Uganda, vikifahamika zaidi kama ‘vita vya Kagera’ 1978/79. Tanzania ilikadiriwa kutumia zaidi ya dola za Kimarekani milioni 1, sawa na zaidi ya Tsh bilioni 1 kwa kila siku ya vita, katika vita ambavyo vilidumu kwa karibu mwaka mzima.
Nguvu kazi ya Taifa ilipotelea humo kwa vifo na majeraha, huku pia mali zikiteketea, vyakula kukusanywa kutoka maeneo mbalimbali na kupelekwa kwenye ukanda wa vita, mashamba na barabara kuharibiwa na pia kusimama kwa shughuli za msingi za maendeleo ya Taifa.
Huu ulikuwa mkasa mkubwa kwa historia ya Taifa la Tanzania, na kwamba hali ya uchumi ilidorora kiasi kilichomfanya muasisi wa Taifa kuunda tena upya mikakati ya kuinusuru nchi na hasara iliyoingia.
Si hivyo tu, baada ya majanga hayo makuu matatu hali nyingine pevu iliendelea kulisakama Taifa na safari hii ilikuwa njaa kuu iliyotokana na ukame mkubwa katika miaka ya 1980.
Wananchi walitaabika na kuchoshwa na hali ile, lakini sera na mipango rafiki ya Mwalimu Julius Nyerere huku akiungwa mkono vyema na wazalendo waliotambua na kuielewa nia yake kwa Taifa, walivuka kizuizi na kusonga mbele.
Sasa Tanzania imeingia katika ulimwengu mpya wa utandawazi tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990, huku utandawazi huo pia ukipenya ndani ya nguzo za uongozi wa Taifa na uhuru kuwaghubika watawala baada ya miiko ya uongozi iliyosimikwa na baba wa Taifa katika Azimio la Arusha kuvunjwa na kuwekwa kapuni.
Mwendo wa maendeleo umepungua, japo kasi ya matumizi ya rasilimali za Taifa imeongezeka mara dufu kwa kulinganisha na nyakati za Nyerere aliyependelea elimu kwanza kwa wananchi kabla ya kuanzisha matumizi hayo.
Kilichotarajiwa na wengi katika enzi hizi, ni kuongezeka kwa kuboreshwa na kuongezeka kwa vitu alivyoanzisha muasisi wetu kama vile shule, hospitali, barabara, viwanda, majosho, mashamba makubwa ya kisasa, miundombinu ya maji, nishati ya umeme, huduma nyingine za kijamii pamoja na kukua kwa awamu kwa hali ya maisha ya wananchi.
Pengine kwa jicho la harakaharaka kama inavyosemekana hivi sasa, ni kwamba baadhi ya vitu hivi vimeongezeka. Lakini itambulike kuwa kilichokuwepo wakati wa Nyerere angalau kilikuwa kikiwatosheleza watu wa wakati huo kwa idadi kama yao, na kila walipoongezeka zaidi, huduma pia zililazimika kuongezeka.
Sasa tumejisahau na kujiona kuwa na barabara zaidi ya wakati ule, shule na hospitali. Lakini zinalingana na idadi ya watu wa sasa?
Kwa sababu hapa katikati tangu Mwalimu aachie madaraka, hakuna janga kubwa lililowahi kulikumba Taifa kama yale ya mgogoro wa mafuta duniani (1973) na vita vya Kagera. Hivyo kwa mapenzi mema na utashi wa viongozi walioibeba nchi baada ya Nyerere, kulikuwa na haja ya kupanda siku baada ya siku hadhi ya mwananchi wa kawaida.
Madini yametumika kinyume na malengo, na mapato ya mazao ya misitu, kodi za wananchi, mazao ya bahari, utalii na vinginevyo vimekumbwa na mirija inayohamishia utajiri kwa watu binafsi, na mfumo mzima wa kunufaisha jamii nzima umeharibiwa.
Zamani wakulima walipata mbolea na pembejeo bure na kupewa wataalamu wa kilimo huku pia maghala makubwa yakijengwa kuhifadhi mazao yao, zikiwemo pia hifadhi, mashine na viwanda vya kukoboa nafaka katika maeneo makubwa ya uzalishaji (National Milling), sambamba pia na Vyama vya Ushirika kuwasaidia wakulima katika maslahi yao na mwendelezo wa kilimo. Suala la kustaajabu, badala ya vitu hivi kuboreshwa na kuongezeka, vimekufa na maghala yale na viwanda vimekuwa magofu.
Hali kadhalika, kwa upande wa wafugaji, majosho mengi yalijengwa kutunza afya za mifugo, na huduma hii ilisimamiwa kikamilifu na Serikali na ilitolewa bure.machinjio makubwa yalijengwa kuvuna mazao ya mifugo hiyo ikiwemo kusindika nyama na kuuza, kutumia ngozi kutengezea bidhaa mbalimbali na kutengeneza mbolea. Hivi sasa, vitu hivyo havipo tena, na kama vipo basi ni vya watu binafsi wanaohesabika na si vya umma tena.
Viwanda ni ijini nyingine ya ukuaji wa Taifa, na miaka iliyopita viwanda kadha vilijengwa katika maeneo mbalimbali kuendana na uzalishaji wa eneo hilo. Kwa mfano viwanda vya nguo (Textiles) vilijengwa sana katika mikoa ya uzalishaji wa pamba, viwanda vya kutengeneza bidha za mazao ya katani, sukari, kusindika samaki, simenti, mabati, mbolea, zana za kilimo kama vile majembe, viwanda vya chai, kutengeneza karatasi kutokana na mbao na vingine vilijengwa nchini, lakini hivi vilikufa baadaye.
Mashirika ya umma yalianguka, na hakukuwa na misingi thabiti iliyochukua kazi yake kuwanufaisha wananchi kufidia kazi iliyofanywa na mashirika hayo, na matokeo yake ndio haya wananchi walio wengi kutaabika, huku wale waliopata fursa ya kutumia kilichopatikana wakajenga tabaka lao linalotofautiana na wengi wa wananchi wa sasa.
Na ni nini cha kufanya baada ya yote haya tena baada ya miaka 50 ya uhuru wetu? Suala la msingi ni kuungana tena pamoja tuweke uzalendo mbele. Tusishangilie hatua tuliyofikia, bali tujikosoe kwa mabaya tuliyofanya na kujikwamisha wenyewe, tutunge mbinu za kulijenga Taifa kwa usawa.

 
image
image
This text will be replaced
image