Siku ya Mwalimu Nyerere, tukumbuke pamoja
Nguzo iliyoshikilia matawi tuliyokaa sisi ilimeguka na kusinyaa ghafla na machozi yakatanda huku giza nalo likienea na kujaa, maana tulijua harudi tena; ni Oktoba 14, mwaka 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas Uingereza, wakati huo Mzee Mkapa akiongoza Taifa. 
Hakuna aliyetegemea shujaa kama yule angeondoka tena kwa wakati kama ule, tukiwa hata hatujafikiri nini kijacho baada yake, huku Taifa likikabiliwa na changamoto nzito za utandawazi, na kila mmoja akiwa hana ufunguo wa kuingia.
Mwalimu alikuwa ameona mizizi yake na jinsi ilivyokuwa ikitanda na kuenea, hasa kwa nchi changa na alitambua uchungu wa sumu yake pindi tukakapoitafuna. Nani alijua wapi tungepita nyakati hizo kama angekuwepo na angeshauri kipi na kingetufaa vipi.
Kuna msemo katika maandiko unaosema “alivunja la kwanza ili aweze kusimika la pili”, na hapa Mwalimu amekuwa mfano dhahiri kwa kuwa ndiye mfano wa kwanza pekee barani Afrika kujikana na kujivua madaraka na mamlaka yake, ili mbegu nyingine zichipuke kuendeleza msingi. Lakini alikuwa nyuma akitazama na alionyesha kidole kuashiria mwelekeo sahihi.
Taifa lilisimama na kujitambulisha miongoni mwa Mataifa ya ulimwengu, na tukajenga taswira yetu peke yetu yenye uzuri usio kifani na kutamaniwa mithili ya mali asili ya mbuga, milima, mito, historia na uoto wa asili unaovutiwa na wageni wengi pote duniani.
Miongoni mwa misingi hiyo ni kile ambacho kimekuwa kikisimuliwa kila kukicha, amani; kisha umoja ulioundwa kwa kuvunjwa kwa kuta za makundi ya asili, makabila na koo mbalimbali, kufungua mlango wa muingiliano uliotanda kama maziwa yaliyochanganywa katika chai na kukolea.
Misingi ya utawala bora ilisimikwa, kuandikwa katika vitabu na kusomwa hata na watoto wanaozaliwa na kuingia katika madarasa ya awali, kutambua dhamana ya nchi, dhamana ya cheo, huduma kwa Taifa, usawa wa kila nafsi na siri ya kupambana na maadui wa maendeleo.
Njia tuliiona, mbele tukatazama na hatua zikapigwa. Lakini je, tuko wapi? Ile njia bado tunaiona? nani amesimama katika mstari tuliochorewa na kudumisha viapo vilivyoandikwa.
Ni wazi kuwa yaliyoandikwa yameandikwa, na yanayotendwa yanatendwa, hakuna ubishi wala hakuna cha kujiuliza kwa kuwa kila jambo liko wazi.
Hivi sasa ishara zimeondoka, na njia zilizokuwa zikituongoza zimeota nyasi na hazionekani tena; mtego uliowekwa kuchunga wanaotakiwa katika kundi na kuepusha wasiotakiwa umekamata wote waliolengwa na waliowekewa vizuizi kwa kuwa kuta zake zilipata majeraha, na sasa tumechanganyika, hatuna wa kusimamia lililo la msingi na haki.
Wakati huu katika maadhimisho ya kumbukumbu yake pamoja na miaka 50 ya uhuru, taarifa zinabainisha mbuzi zaidi ya 20 wamekuwa wakichinjwa Butiama na maeneo ya jirani, vinywaji wa kila aina vikimiminika humo, huku maonyesho mbalimbali ya kumbukumbu yakifanyika.Lakini sherehe na kumbukumbu hizi zaweza kukosa tija iwapo hatutarudi katika misingi inayokubalika aliyoiamini muasisi huyu.
Kwa uthabiti, hatupaswi kuishia hapo, hatuna budi kurudi nyuma tena kwa dhamira kila mmoja kwa ari yake, na hasa kundi la vijana kwa kuwa hata mwalimu alifikiria mabadiliko akiwa kijana, akajipanga na akashika mpini tayari kwa mapambano.
Yote aliyotuachia Mwalimu yakaporomoka, yanaweza kurudi na pale tutakapokuwa na mtazamo sahihi, sauti isiyofaa tutaikana na ile sahihi ikitoka sote tutaitambua na wote tutaifuata na kuiunga mkono. Ni sharti tujenge Taifa lenye mategemeo na kulinda heshima na sura ya utulivu, ubora na uwajibikaji, tukibakia kuwa kisiwa cha amani.
Top Stories »





