Sudan Kusini ruksa EAC, kutumia Kiswahili
Siku chache baada ya Shirikisho la Jumuiya ya Afrika Mashariki kukataa ombi la Serikali ya Sudani Kaskazini kujiunga Jummuiya hiyo, upepo umekuwa tofauti kwa Sudan ya Kusini iliyojipatia uhuru hivi karibuni, baada ya kupata ruksa ya kujiunga. 

Azimio hilo lilifikiwa katika mkutano wa pamoja wa viongozi wa juu wa Mataifa yanayounda Jumuiya ya Afrika Mashariki, katika mkutano uliokuwa ukiendelea nchini Burundi.
Kwa mujibu wa Katibu mkuu Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Stegomena Taksi, Taifa jipya la Sudan Kusini limekuwaliwa kuwa mwanachama wa Jumuiya hiyo baada ya kutimiza vigezo vilivyoainishwa na kwamba taratibu za usajili kamili zinaendelea kufanyika kuipa uanachama kamili.
Itakumbukwa kuwa Serikali ya kuu ya Sudan ikiongozwa na Raisi wake Omari Hassan Albashir iliwasilisha ombi la kutaka uanachama Afrika Mashariki, lakini viongozi hao walitupilia mbali ombi hilo, wakidai kuwa Sudan haijatimiza masharti yaliyotakiwa.
Wakati hilo likijadiliwa, Baraza la viongozi hao pia limeazimia kuanzisha Kamisheni ya Lugha ya Kiswahili itakayokuwa na makao yake makuu mjini Zanzibar, kwa ajili ya kuratibu na kuendesha shughuli za lugha hiyo, iliyokubaliwa kuwa lugha rasmi ya kutumika ndani ya Jumuiya hii.
Lugha ya Kiswahili imepewa kipaumbele kutumika katika ukanda huu, hasa ikizingatiwa kuwa jamii nyingi za ukanda huu zinatumia lugha hiyo pamoja na lugha nyingine ya Kimataifa, kama ilivyo Kenya, Tanzania na Uganda wanaotumia Kiswahili na Kiingereza, huku Rwanda na Burundi wakitumia Kifaransa na Lugha za nyumbani, lakini baadhi ya wananchi wake pia huzungumza Kiswahili.
Kwa upande mwingine Katibu Stigomena amebainisha kuwa Serikali ya Tanzania imekataa kusaini baadhi ya makubaliano ya Jumuiya hiyo yaliyojadiliwa katika mkutano huo wa Bujumbura Burundi, baada ya kutoridhishwa nayo likiwemo suala la ‘Ulinzi na usalama’ kwa nchi wanachama.
Top Stories »





