TFF yawafuta kazi waamuzi 3 na kamishna
Shirikisho la kandanda nchini TFF leo limewaondosha Waamuzi watatu na kamishna mmoja katika majukumu yao ya kuchezesha na kusimamia mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kutokana na kuonyesha upungufu katika uchezeshaji na usimamizi. 

Uamuzi huo ulifanywa na Kamati ya Ligi iliyokutana jana (Februari 11
mwaka huu) ambapo pamoja na mambo mengine ilipitia taarifa za waamuzi
na makamishna wa VPL ambayo leo (Februari 12 mwaka huu) inaendelea
katika raundi ya 17.
Peter Mujaya wa Mwanza aliyechezesha mechi namba 101 kati ya JKT Ruvu
Stars na Yanga amefungiwa kwa miezi 12 kwa mujibu wa Kanuni ya 26(a)
ya Ligi Kuu ya Vodacom kwa kushindwa kumudu mchezo huo, hivyo kupata
alama za chini.
Naye Isihaka Shirikisho wa Tanga ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi
wa VPL msimu huu kwa kushindwa kumudu mchezo namba 105 kati ya Simba
na JKT Oljoro. Moja ya udhaifu alioonesha ni kushindwa kumuadhibu
mchezaji Patrick Mafisango ambaye alimsukuma baada ya kumuonesha kadi
nyekundu Haruna Moshi wa Simba.
Mwamuzi mwingine aliyefungiwa kwa miezi 12 kwa mujibu wa Kanuni ya
26(a) ni Kennedy Mapunda wa Dar es Salaam aliyechezesha mechi namba
107 kati ya Villa Squad na Simba. Moja ya udhaifu wa Mapunda ni
kushindwa kumpa kadi nyekundu Fred Cosmas wa Villa Squad baada ya
kumuonesha kadi ya pili ya njano.
Pia waamuzi wasaidizi Michael Mkongwa wa Iringa na Kudura Omary wa
Tanga waliochezesha mechi namba 112 kati ya Yanga na Mtibwa Sugar
wameondolewa katika mechi zilizobaki za VPL kwa kutokuwa makini.
Mwamuzi wa mechi hiyo Ibrahim Kidiwa amepewa onyo.
Waamuzi wengine waliopewa onyo na kutakuwa kujirekebisha ni Hashim
Abdallah wa Dar es Salaam aliyechezesha mechi namba 92 kati ya Moro
United na Yanga, na mwamuzi msaidizi wa mechi ya Simba na Coastal
Union, Issa Malimali wa Ruvuma.
Kamishna wa mechi namba 112 kati ya Yanga na Mtibwa Sugar, Mohamed
Nyange ameondolewa katika orodha ya makamishna kwa mechi zilizobaki za
VPL kutokana na ripoti yake kuwa na upungufu.
Wakati huo huo
Kamati ya Ligi imeagiza mchezaji Patrick Mafisango wa Simba aandikiwe
barua ya onyo kutokana na kumsukuma mwamuzi Isihaka Shirikisho baada
ya kumuonesha kadi nyekundu mchezaji mwenzake Haruna Moshi kwenye
mechi kati ya Simba na JKT Oljoro.
Nayo klabu ya Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 baada ya washabiki
wake kurusha makopo ya soda na chupa za maji wakipinga uamuzi wa
mwamuzi Shirikisho kumtoa kwa kadi nyekundu Haruna Moshi.
Wachezaji waliopigwa faini ya sh. 500,000 kila mmoja baada ya
kuoneshwa kadi nyekundu kutokana na kupiga ambapo pia wanakosa mechi
tatu za ligi kwa mujibu wa Kanuni ya 25 ni nahodha wa Yanga, Shadrack
Nsajigwa na Cyprian Lukindo wa Villa Squad.
Aidha, TFF imetangaza mapato baina ya vilabu vya Simba na Azam iliyochezwa hivi karibuni, ambapo kiasi cha Tsh milioni 67 zimepatikana kutokana na mpambano huo wa
Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Azam uliochezwa
Februari 11 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Jumla ya watazamaji 19,257 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo namba
117 kwa kiingilio cha sh. 3,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 15,000
kwa VIP A.
Baada ya kuondoa gharama za awali za mchezo na asilimia 18 ya Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 10,303,932.20 kila timu
ilipata sh. 13,182,800.34, uwanja sh. 4,394,266.78.
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh.
1,757,706.78, TFF sh. 4,394,266.78, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa
Miguu (FDF) sh. 2,197,133.39, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh.
439,426.78 na asilimia 10 ya gharama za mechi ni sh. 4,394,266.78.
Gharama za awali za mechi zilikuwa nauli ya ndani kwa waamuzi sh.
10,000, nauli ya ndani kwa kamishna wa mchezo sh. 10,000. wamuzi wa
akiba sh. 30,000, tiketi sh. 4,350,000, maandalizi ya uwanja (pitch)
sh. 400,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi kwa uwanja sh.
2,350,000 na Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000.
Gharama nyingine ni Jichangie ambayo ni sh. 200 kwa kila tiketi; kila
klabu ilipata sh. 1,347,990,280 wakati Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa
wa Dar es Salaam (DRFA) kilipata sh. 1,555,420.
Top Stories »





