Yafahamu maajabu ya bwawa la Kinondoni
Kata ya Kinondoni imegawanyika katika mitaa minne ya Kinondoni Shamba, Kinondoni ADA Estate, Kinondoni Mjini pamoja na ule wa Kinondoni Block 41 ambao ndio wenye bwawa hili lisilodhaniwa na wengi. 

Wilaya ya Kinondoni katika jiji la Dar es Salaam imegawanyika katika kata zipatazo 27, mojawapo ikiwa kata ya Kinondoni kitovu cha wilaya hiyo, pamoja na Magomeni, Makurumla, Ndugumbi, Tandale, Mwananyamala, Msasani, Mzimuni, Kigogo, Mabibo, Manzese, Ubungo, Kibamba, Goba, Kawe, Kunduchi, Mbweni, Bunju, Makuburi, Mburahati, Makumbusho, Sinza, Kijitonyama, Kimara, Mbezi, Mikocheni na Hananasif.
Ikiwa na ukubwa wa km2 531 na wakazi zaidi ya 1,088,867 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002, wilaya ya Kinondoni ina baadhi ya mito na inapakana pia na ukanda wa bahari, kama vile rasi ya Msasani Kunduchi hadi Mbweni.
Ukiwa katikati ya mji, ikitajwa “Kinondoni” basi wazo la kwanza kuja kichwani ni kata maarufu ya Kinondoni kitovu cha wilaya hiyo ambayo ndiyo tutakayoizungumzia na bwawa lake, ikianzia katika eneo la Kwa Manyanya katika barabara ya Kawawa kwenda katika uwanja wa Biafra hadi Morocco, kisha kushuka kupitia kituo cha Mbuyuni katika barabara ya Al Hassan Mwinyi, Ubalozi wa Ufaransa na tena hadi daraja la Selander na kupanda kupitia barabara ya Kinondoni inayoanzia Selander kupitia kituo cha basi cha Mwembeni hadi Manyanya tena.
Kata ya Kinondoni imegawanyika katika mitaa minne ya Kinondoni Shamba, Kinondoni ADA Estate, Kinondoni Mjini pamoja na ule wa Kinondoni Block 41 ambao ndio wenye bwawa hili lisilodhaniwa na wengi.
Maajabu ya kwanza ni kusikia kuwepo kwa bwawa katika eneo hili la kati la Manispaa ya jiji, lenye msongamano wa watu wengi.
Pamoja na uwepo wa bwawa hili kwa miaka mingi, halijulikani kabisa na watu wengi ukiacha tu wale majirani wanaolizunguka.
Kutokujulikana kwake, kunatokana na kuzungukwa na makazi ya watu katika kuta zinazozuia mwonekano wake.
Kitu kingine kinacholificha bwawa hili ni kuwa hata ukifanikiwa kulifikia unaweza usitambue kama ni bwawa, kwa vile utakutana tu na taswira ya kijani kibichi kinachovutia, mithili ya uwanja mzuri wa mpira tambarare kabisa.
Bwawa hili linalokadiriwa kuwa na urefu m2 2500, limetanda magugu maji juu yake, karibu kabisa na mpaka kati ya mtaa huo wa Block 41 na ule wa ADA Estate.
Nilipolitembelea bwawa hili kwa mara ya pili mnamo June 6 mwaka 2010, nikiambatana na Mwenyekiti wa mtaa huo Bwana Majeshi, kama kawaida nililakiwa na kijani kibichi, kisha pembeni akaonekana mnyama hatari wa majini.
Chanzo cha maji yake ni nini?
Ni vigumu kutambua chanzo cha maji ya bwawa hili kutokana na mazingira lilipo na kwamba maji yake yanadumu hata nyakati za kiangazi mwaka mzima.
Pengine utafiti zaidi unapaswa kufanyika kugundua zaidi. Lakini kwa mujibu wa baadhi ya majirani, hasa wale wazee ambao wamekuwa wakilifahamu tangu kale, moja ya sababu ya kuwepo maji hayo ni mtiririko wa maji kutoka maeneo mbalimbali nyakati za mvua.
Nini kilichopo ndani yake?
Mamba: ndani ya bwawa hilo kuna viumbe hai, na mmoja wao ni mnyama wa majini Mamba ambaye anaonekana kwa umbali katika picha ndogo.
Mamba huyo amedumu kwa muda na inasadikika kuwepo wengine ndani yake, na anaonekana kupata mahitajin yake yote humo kwani tunaambua Mamba ni mwindani, hivyo chakula chake kikubwa ni nyama na bila shaka anawinda wanyama wenziwe ndani ya bwawa.
Samaki: pamoja na Mamba huyo wanaonekana pia samaki lukuki wakubwa aina ya Kambale wakirukaruka kutoka chini ya maji hadi juu ilihali upande wa pili wa bwawa hilo ndiko kwenye maskani ya Mamba.
Kwa mujibu wa majirani wa eneo hilo pamoja na Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo, hakuna madhara yoyote yaliyowahi kuripotiwa kutokana na Mamba huyo, na hakuwahi kuonekana akizurura mitaani, jambo linaloonyesha maisha yake ni kwenye maji hayo tu na anapotoka anaota jua kandokando ya bwawa.
Top Stories »





