Wakati Jumuiya ya Kiislamu nchini ikijiandaa kwa sikukuu ya Eid El Fitri kesho Ijumaa baada ya mwezi kuandama jioni hii, shambrashambra za kusheherekea siku hiyo kwa kupiga fataki juu zimepigwa marufuku huku Jeshi la Polisi likitoa angalizo kwa suala zima la usalama.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa kanda maalumu ya Dar es Salaam Suleiman Kova, katazo hilo limetolewa kuepusha rapsha zozote zinazoweza kutokea kutokana na milipuko ya fataki hizo.
Kadhalika Kamanda Kova amewataka wazazi wote kuhakikisha usalama wa watoto wao kwa kutowaacha kutembea njiani bila uangalizi na kuonya juu ya kutoka majumbani na kuacha bila ulinzi thabiti kuepusha wizi unaoepukika.
Aidha mkuu huyo wa polisi amewaonya madereva wa daladala kote jijini katika kubeba abiria kupita kiasi pamoja na kuepuka kutumia magari ya wazi kama Canter na Malori kubebea abiria.